UTAFITI: MABAKI YA MKONGE YAZALISHA MBAO, MBOLEA, VYAKULA VYA MIFUGO NA NISHATI MBADALA

Imewekwa: 23 Oct, 2026
UTAFITI: MABAKI YA MKONGE YAZALISHA MBAO, MBOLEA, VYAKULA VYA MIFUGO NA NISHATI MBADALA

Utafiti uliofanywa na watafiti wanne kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kupitia Mradi wa Agroval umebaini kuwa mabaki ya mkonge yanaweza kuongezwa thamani na kutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali, zikiwemo mbao za ujenzi, mbolea, protini kwa ajili ya vyakula vya mifugo na nishati mbadala, ikiwemo biogesi.

Mradi huo unalenga kuongeza thamani ya mabaki ya mazao mbalimbali, hususan Mkonge na kahawa, kwa kuangalia fursa zake katika nyanja za kiuchumi, kilimo, ufugaji, mazingira na maendeleo ya jamii.

Watafiti waliohusika katika utafiti huo ni Dk. Clemence Ansbert (Biocomposite), Selemani Said (Biogas), Nickson Kahigi (Life Cycle Analysis) na Dk. Aziza Konyo (Black Soldier Fly Larvae).

Akizungumza baada ya kuwasilishwa kwa matokeo ya awali ya utafiti huo jijini Tanga, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona, amesema kwa muda mrefu Bodi imekuwa na matarajio ya kuona tafiti za aina hiyo zikifanyika na kutoa matokeo yatakayosaidia kuongeza thamani ya zao la mkonge.

Amesema kwa sasa uzalishaji umejikita zaidi katika singa za mkonge, ambapo takribani asilimia 70 ya singa hizo huuzwa nje ya nchi. Hata hivyo, singa hizo zinawakilisha takribani asilimia mbili hadi nne tu ya mmea mzima wa mkonge, huku sehemu kubwa ya mabaki yake yakitupwa kama taka.

“Sasa watafiti wamekuja kuangalia kama yale mabaki yanayotupwa kama uchafu yana manufaa yoyote katika kujenga uchumi wa nchi. Matokeo ya utafiti huu yameonesha kuwa mabaki ya mkonge yanaweza kutumika kuzalisha mbao kwa ajili ya ujenzi, mbolea kwa matumizi ya kilimo, pamoja na umeme, joto na gesi kwa matumizi ya nishati mbadala (biogesi).

“Pia, mabaki hayo yanaweza kutumika katika uzalishaji wa uyoga na nzi chuma (Black Soldier Fly) kwa ajili ya kuzalisha protini inayotumika katika vyakula vya kuku na mifugo mingine, wakiwemo ng’ombe,” amesema Kambona.

Ameongeza kuwa Bodi imefurahishwa na matokeo hayo ya awali na inatarajia kupokea wasilisho la pili litakalokuwa na matokeo zaidi. Amesema kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Bodi inapanga kuandaa mkutano mkubwa utakaowakutanisha wadau ili kuwafahamisha matokeo ya utafiti huo na fursa za uwekezaji zinazotokana na mabaki ya mkonge.

Amesema hatua hiyo itawawezesha wadau kufanya maamuzi ya uwekezaji kwa kutumia takwimu na matokeo ya utafiti badala ya kubahatisha, huku wakibaini namna wanavyoweza kunufaika na zao la mkonge katika maeneo mbalimbali.

Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela na Mtafiti Kiongozi wa mradi huo, Profesa Anthony Mshandete, amesema utafiti huo umefanyika kwa ushirikiano wa nchi nne ambazo ni Tanzania, Kenya, Ethiopia na Denmark, na kufadhiliwa na Shirika la Danida la Denmark.

Amesema Tanzania ilijikita zaidi katika kuongeza thamani ya mabaki ya mkonge, ambapo watafiti walifanikiwa kutengeneza mbao mbadala wa mbao za kawaida zinazotokana na miti. Pia, walichunguza uendelevu wa teknolojia zilizobuniwa kupitia mradi huo.

“Tumegundua kuwa tunahitaji kuangalia athari za kimazingira za kila teknolojia na kubaini mambo ambayo mwekezaji anapaswa kuzingatia kabla ya kuwekeza.

“Pia, katika kuboresha matumizi ya mabaki ya mkonge, tumegundua kuwa kuyachanganya na mabaki mengine ya kilimo kunaboresha uzalishaji wa biogesi, ambayo ni sehemu ya uchumi wa kijani na inachangia upatikanaji wa nishati salama na rafiki kwa mazingira,” amesema Profesa Mshandete.

Naye Dk. Clemence Ansbert, ambaye utafiti wake ulihusisha utengenezaji wa mbao kwa kutumia nyuzi zinazotokana na mabaki ya mkonge, amesema teknolojia hiyo itasaidia kupunguza matumizi na utegemezi wa mbao zinazotokana na miti.

Amesema matumizi ya mbao hizo yanaweza kuchangia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuunga mkono azma ya kuwa na Tanzania ya kijani, kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Mbao hizi zinaweza kutumika katika matumizi mbalimbali ya ujenzi ambayo hayahitaji uwezo mkubwa wa kubeba mizigo. Pia, zina uimara wa kutosha, hazibadiliki rangi wala kuruhusu maji kupenya,” amesema Dk. Ansbert.

Kwa upande wake, Dk. Aziza Konyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amesema utafiti wake ulilenga kutafuta suluhisho la tatizo la uzalishaji mkubwa wa taka katika viwanda vya mkonge.

Amesema katika uzalishaji wa singa za mkonge, ni takribani asilimia nne hadi sita tu ya mmea inayotumika kupata singa, huku sehemu kubwa iliyobaki ikiwa ni mabaki ambayo mara nyingi hutupwa kama taka.

“Katika utafiti wangu, nilitumia mabaki hayo kuzalisha protini na mbolea isiyo na kemikali kwa kutumia teknolojia ya nzi chuma (Black Soldier Fly).

“Katika mnyororo wa kuongeza thamani ya mabaki ya mkonge, lava wa nzi chuma hutumia mabaki hayo kama chakula ndani ya siku 10 hadi 14. Baada ya hapo, lava hao huvunwa, kukaushwa na kutumika kama chanzo mbadala cha protini badala ya soya au dagaa katika utengenezaji wa vyakula vya mifugo.

“Baada ya lava kutumia mabaki hayo, kiasi kinachobaki ambacho hakijaliwa hutumika kutengeneza mbolea nzuri isiyo na kemikali,” amesema Dk. Konyo.

Taasisi Shirikishi
Hakimiliki ©2026 Bodi ya Mkonge Tanzania. Haki zote zimehifadhiwa.