TSB YATOA UFAFANUZI CHANGAMOTO SEKTA YA MKONGE

Imewekwa: 27 Jan, 2025
TSB YATOA UFAFANUZI CHANGAMOTO SEKTA YA MKONGE

Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), imetoa ufafanuzi kuhusiana na habari zilizochapishwa kwenye baadhi ya magazeti ambayo yalihusisha sekta hiyo hususani wakulima wadogo wa zao la Mkonge.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Tanga, Mkurugenzi Mkuu wa TSB, Saddy Kambona amesema magazeti hayo yalichapisha taarifa kuhusu Vyama vya Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) vya Hale, Magoma, Magunga, Mgombezi na Mwelya vilivyopo Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

Ameyataja magazeti ya Raia Mwema la Julai 24-30 ambalo lilichapisha makala yenye kichwa cha habari 'Kinachoendelea kwenye Mkonge, utamwaga machozi', Julai 26-30 gazeti la Tanzania Leo lilichapisha makala 'Kinachoendelea kwenye Mkonge ni ukatili kwa wakulima: Serikali iingilie kati gharama za usindikaji na julai 30-Agosti 5 gazeti la Jamhuri lilichapisha kichwa cha habari 'Bashe 'ishu' ya Mkonge unaiweza'.

Mkurugenzi Kambona amesema mambo yaliyoguswa na magazeti hayo ni Kampuni ya Sisalana kupandisha bei ya huduma ya uchakataji kutoka Sh milioni moja kwa tani hadi Sh milioni 1.25  kwa tani, uchakavu wa mitambo ya uchakataji wa Mkonge yanayomilikiwa na Kampuni ya Sisalana (T) Ltd unaosababisha hasara kwa wakulima.

Nyingine ni ununuzi wa Mkonge na changamoto zake na suala la umiliki wa Makorona baina ya NSSF na AMCOS kwa uwiano wa asilimia 60 na asilimia 40 mtawalia.

UFAFANUZI:

Mkurugenzi Kambona amesema kuhusu hoja ya Kampuni ya Sisalana ni kweli Juni 13, mwaka huu bodi ilipokea nakala ya barua yenye Kumb.Na.STCL/AMCOS/VOL I/42 kwenda AMCOS yenye kichwa cha habari “Maboresho ya utendaji wa Kampuni”.

“Kwenye maelezo ya barua hiyo kampuni ya Sisalana ilizungumzia, pamoja na mambo mengine, kusudio la kufanya maboresho ya bei na kueleza kuwa inapendekeza bei iwe Sh 1,225,000 kwa meta 35 kwa tani ambapo TSB ilisubiri majibu ya Amcos kuhusiana na hoja za Kampuni ya Sisalana,” amesema.

Amesema Julai 15, mwaka huu AMCOS waliandika barua kwa TSB kuomba muongozo wa bei ya usindikaji baada ya kupokea hati za madai ya malipo (Invoices) zenye bei mpya ya usindikaji. TSB ilielekeza uongozi wa AMCOS kutolipa ankara hizo hadi suala hilo litakapofanyiwa kazi na kuamuliwa kwa pamoja baina ya TSB, Kampuni ya Sisalana, Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Tanga na AMCOS na Juni 14, mwaka huu TSB ilikutana na Kampuni ya Sisalana na Julai 30 ilikutana na AMCOS kujadili suala hili.

“Nichukue fursa hii kuwaeleza wakulima wadogo wa Mkonge wa Korogwe pamoja na AMCOS kutulia kwani suala hili tunalifanyia kazi. Tutakuwa na kikao cha dharura Agosti 2, baina ya TSB, Sisalana, Mrajis Msaidizi wa Tanga na AMCOS.

“Kutokana na hali hiyo, ni vyema wadau wote wa sekta ndogo ya Mkonge kujizuia na kutokuzua migogoro inayoweza kuzua taharuki katika kipindi hiki tunacholekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo utulivu ni jambo muhimu sana. Tufuate taratibu na kushirikishana,” amesema Mkurugenzi Kambona.

Aidha, kuhusu uchakavu Makorona yanayomilikiwa na Sisalana (T) Ltd unaosababisha hasara kubwa kwa wakulima wa Mkonge Mkurugenzi Kambona amekiri kuwa kuwa mitambo ya uchakataji wa Mkonge iliyopo kwenye mashamba ya Hale, Magoma, Magunga, Ngombezi na Mwelya ambayo inamilikiwa na Kampuni ya Sisalana ni mitambo ya zamani lakini ni ukweli usiopingika kuwa mitambo hiyo ni mitambo bora na yenye ufanisi mzuri katika kuzalisha singa bora kuliko sehemu kubwa ya mitambo ya kisasa.

“Hii ndiyo sababu makampuni yote makubwa ya Mkonge kama vile Amboni Plantations Ltd, Mohamed Enterprises Ltd, Highland Estates Ltd, SFI yanatumia makorona sawa na hayo ya Sisalana. Tofauti ni matunzo, usimamizi wa mitambo hiyo na uendeshaji wake.

“Mitambo ya Sisalana ikifanyiwa matengenezo vizuri kama inavyofanyika kwa makampuni ya wakulima wakubwa na kuiweka katika ulingano sawa (setting) ina uwezo wa kufanya vizuri zaidi na kupunguza hasara ya kutupa shimoni singa za wakulima. Hivyo tatizo sio makorona ila tatizo ni usimamizi mbaya na uendeshaji mbaya wa mitambo hiyo chini ya Kampuni ya Sisalana.

“Natoa wito kwa Kampuni ya Sisalana Company Limited kufanya matengenezo ya haraka ya mitambo yake hasa shamba la Magoma, Mwelya na Ngombezi (kwa sasa) kwa kuwa hali ya mitambo katika mashamba ya Hale na Magunga ina nafuu,” amesema Mkurugenzi Kambona.

Pamoja na mambo mengine, akizungumzia suala la ununuzi wa Mkonge na changamoto zake amesema tangu mwaka 2021 mnunuzi wa Mkonge wa AMCOS tano za Korogwe alikuwa ni Kampuni ya Mohamed Enterprises Ltd (MeTL) ambaye alinunua Mkonge kwa miaka mitatu mfululizo hadi Mkataba wake ulipofika mwisho Agosti mwaka jana.

Amesema mazungumzo ya kuongeza mkataba yalishindikana kwa sababu ya ofa ndogo ya bei iliyotolewa na kampuni ya MeTL ambapo kampuni hiyo ilitaka kupunguza bei kwa tofauti ya Sh 600,000 kwa daraja la UG yaani kutoka Sh milioni 3.7 hadi Sh milioni 3.1 na baadaye waliishia Sh milioni 3.3 kwa tani.

“Baada ya mazungumzo baina ya AMCOS, TSB na MeTL kushindikana, TSB iliitisha zabuni ya ununuzi wa Mkonge ambapo Kampuni ya WEFARMTZ ilishinda zabuni kwa bei ya Sh 3,900,000 na kuanza kununua Mkonge wa Amcos hadi Aprili 22, mwaka huu ambapo mkataba baina ya AMCOS na WEFARMTZ ulivunjika kutokana na ukiukwaji wa vipengele vya mkataba.

“Baada ya kuvunjika kwa mkataba huo, Mshindi wa pili wa Zabuni ya ununuzi ambaye ni Kampuni ya Agriculture Fibers ilisaini mkataba wa ununuzi wa singa tarehe 22 Aprili, 2024 kwa bei za mshindi wa kwanza.

“Kampuni hiyo inaendelea na ununuzi wa Mkonge kwa sasa. Ni ukweli kwamba kipindi cha miezi takriban miezi tisa tangu Agosti mwaka jana mkataba wa MeTL ulipomalizika, kilikuwa ni kipindi kigumu. Hata hivyo TSB kwa kushirikiana na AMCOS na Wizara ya Kilimo hasa kwa maelekezo ya Mheshimiwa Hussein Bashe tumepambana kutetea maslahi ya mkulima mdogo wa Mkonge kwa kulinda bei ya Mkonge isiporomoke.

“Serikali inatumia nguvu nyingi kukuza kilimo cha Mkonge. Bei nzuri ya Mkonge ni kivutio muhimu. Hatuwezi kuruhusu jitihada za Serikali za kuongeza uzalishaji wa Mkonge kufikia tani 120,000 ifikapo Mwaka 2025/2026 zikwamishwe kwa kuweka mazingira ya kuwakatisha wakulima tamaa ya kuendeleza kilimo cha Mkonge. Kilimo ni biashara na tutahakikisha mkulima mdogo wa Mkonge ananufaika.

Pamoja na mambo mengine Mkurugenzi Kambona amesema suala la umiliki wa makorona baina ya NSSF na AMCOS kwa uwiano wa asilimia 60 na 40 mtawalia amesema ni kweli kwamba ipo hoja ya wakulima wadogo kuhusu suala hili ambayo ilianza kufanyiwa kazi tangu mwaka 2021/2022 ambapo TSB, AMCOS pamoja na Sisalana walikutana na Msajili wa Hazina kujadili suala hili ambayo msingi wa hoja hiyo ya AMCOS ni maelekezo ya Serikali kupitia Waraka wa Baraza la Mawaziri Na.31/2005 kuwa Makorona yaliyopo Hale, Magoma, Magunga, Mwelya na Ngombezi yamilikiwe kwa pamoja baina ya Kampuni ya Katani Ltd na wakulima wadogo.

“Kampuni ya Katani Ltd iliagizwa kuanzisha kampuni kwenye kila shamba ambayo kampuni hiyo ndiyo ingemiliki makorona hayo kwa mgao wa hisa wa asilimia 60 Katani Ltd na asilimia 40 wakulima wadogo (Amcos). Hivyo ilipaswa kuwe na kampuni tano yaani kwenye kila shamba kampuni moja (Hale, Magoma, Magunga, Ngombezi na Mwelya).

“Mwaka 2007 kwenye nyongeza ya mkataba wa mauzo ya hisa za Serikali (addendum) kukawekwa kipengele ambacho kilibadili maelekezo ya Baraza la ambacho kilieleza kuwa hizo hizo asilimia 40 zinapaswa kununuliwa na Amcos na si kupewa (nominal value) kama ilivyoelezwa kwenye waraka wa Baraza la Mawaziri,” amesema.

Taasisi Shirikishi