MAMBO 10 MUHIMU KUHUSU MKONGE
MAMBO 10 MUHIMU KUHUSU MKONGE
Imewekwa: 05 Dec, 2025
Kulinganisha na mazao mengine ya biashara , kilimo cha Mkonge kinafaida nyingi ambazo wengi hawazifahamu, hapa tumekuwekea mambo kumi (10) muhimu ya manufaa ya kilimo cha Mkonge.
- Mkonge huvumilia hali mbaya ya hewa ikiwa ni pamoja na ukame, joto kali au mvua nyingi.
- Hauhitaji pembejeo nyingi, hivyo unaweza kuzalishwa kwa gharama ndogo.
- Magonjwa ya Mkonge yapo kwa kiasi kidogo ambayo hayawezi kuua kabisa mmea endapo kanuni bora za kilimo cha Mkonge zitafuatwa. Magonjwa yanayoshambulia Mkonge ni kuoza shina (Bole rot), mistari ya Pundamilia (Zebra), mabaka kwenye majani (Korogwe Leaf Spot) na wadudu wanaoshambulia Mkonge ni wadudu magamba (Scales) na Tembo wa Mkonge (Sisal weevil) ambao pia hawana madhara makubwa na kuwadhibiti ni rahisi.
- Mkonge huvumilia hali mbaya ya utunzaji, mfano ata bila kupalilia kabisa (ingawa haishauriwi hivyo) Mkonge hauwezi kufa kwa asilimia 100.
- Mkonge ni zao linaloweza kuchanganywa na mazao mengine kama vile mahindi, mazao ya jamii ya kunde n.k
- Mkonge unaweza usivunwe kwa wakati unapokomaa bila kuathiri uzalishaji wake kwa kiasi kikubwa.
- Mkonge tofauti na mazao mengine ambayo ubora wake hupungua kadri muda unavyoongezeka yakiwa ghalani nyuzi za Mkonge zinaweza kuhifadhiwa ghalani kwa muda mrefu bila kuathiri ubora wake ili mradi tu zisipate unyevunyevu. Pia hauliwi na wadudu ikiwa utahifadhiwa sehemu kavu na kwa kuzingatia utunzaji wake kwa kuweka mbao chini kabla ya kuweka robota za Mkonge.
- Zao la Mkonge halina msimu. Kilimo cha Mkonge kinaweza kufanyika baada ya msimu wa kilimo cha mazao mengine ya biashara na ya chakula au wakati wowote wa mwaka.
- Kilimo cha Mkonge hakihitaji mtaalamu wa hali ya juu, hivyo mkulima ataweza kukifanya mwenyewe kwa msaada mdogo wa Bwana Shamba.
- Baadhi ya bidhaa za Mkonge zinaweza kutengenezwa kwa mikono popote hata huko huko vijijini mashamba ya Mkonge yalipo. Bidhaa hizo ni Kamba, vikapu, mikoba, mazuria, virago, mapambo ya ukutani n.k na hivyo kuongeza wigo wa ajira na pato hasa kwa wanawake na vijana.








