WEKENI MIKAKATI YA KUDUMU KUJENGA WIGO WA MASOKO

Imewekwa: 01 Dec, 2025
WEKENI MIKAKATI YA KUDUMU KUJENGA WIGO WA MASOKO

Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) ametoa rai kwa Wakurugenzi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Wizara kuhakikisha wanaweka mikakati ya kudumu katika kukuza wigo wa masoko na biashara ili Sekta ya Kilimo izidi kuimarika.

Amesema hayo wakati wa kikao kazi na Wakuu wa Taasisi za Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB); Mamlaka ya afya ya mimea na viuatilifu Tanzania (TPHPA); Bodi ya Chai Tanzania; Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA); Kampuni ya Mbolea Tanzani, tarehe 26 Novemba 2025, jijini Dodoma.

Kwa upande wa Bodi ya Mkonge Tanzania imeelekezwa kufuatilia haraka urejeshwaji wa mali na majengo ya Bodi hiyo ili kuanza kupanua wigo wa kilimo na kibiashara katika zao la Mkonge.

Uku TPHPA, ameielekeza Mamlaka hiyo kushirikiana kwa karibu na wadau kutoka sekta mtambuka kama vile NEMC ili kuwa na mikakati ya kukabiliana na dharura zinapojitokeza ili kuzuia madhara yoyote kwa mazingira na afya za binadamu.

Akiongea kuhusu Kampuni ya Mbolea Tanzania, Waziri Chongolo amesema “ni muhimu Taasisi zifanye kazi katika sura ya Kilimo Biashara ili huduma ziwe zinamfikia mlengwa wa mwisho, yaani mkulima. Na hapo matokeo ya tija yatapatikana na kuongeza mapato ya Taasisi na kipato kwa mkulima.”

Kuhusu mbolea ya ruzuku, Waziri Chongolo amesema TFRA ifanye tathmini ya uwiano kwa wanufaika wa mbolea ya ruzuku hususan wakulima wadogo na wale wakubwa wanaofanya Kilimo Biashara ili kuweka mikakati mizuri ya kumuinua mkulima mdogo.

Kwa kumalizia, Waziri Chongolo amezielekeza Taasisi zote za Wizara ya Kilimo kuwa na timu ya wataalamu wachache wa kuchambua, kutathmini na kushauri Viongozi pale tatizo lolote linapojitokeza ili kuzidi kuleta tija kwa wakulima.

Taasisi Shirikishi
Hakimiliki ©2025 Bodi ya Mkonge Tanzania. Haki zote zimehifadhiwa.