BAJETI YA KIMKAKATI SEKTA YA MKONGE
Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), amewasilisha Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027, Leo tarehe 28 Aprili ,2026 akibainisha vipaumbele vitano vitakavyochochea ukuaji wa Sekta ya Mkonge nchini.
Miongoni mwa vipaumbele hivyo ni ununuzi na usimikaji wa mashine 10 za kuchakata Mkonge (Dikotiketa), zenye uwezo wa kuchakata hadi tani mbili kwa siku, zitakazofungwa katika mikoa sita inayolima Mkonge.
Aidha, ametaja vipaumbele vingine ambavyo vitatekelezwa na Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) ni pamoja na kuanzisha vituo 13 vya ukusanyaji na uuzaji wa Mkonge kwa ajili ya wakulima wadogo na kuweka miundombinu ya uongezaji thamani (brushing na baling) katika mikoa mitatu, kukamilisha ujenzi wa ghala, ofisi na miundombinu ya maji taka katika viwanda vya Taula na Kibaranga vilivyopo katika Halmashauri za Wilaya za Handeni na Muheza.
“Bodi itakamilisha malipo ya mashine saba za kuchakata Mkonge zinazomilikiwa na Kampuni ya Sisalana katika mashamba matano na kuhamasisha wakulima na kuongeza uzalishaji kutoka tani 64,321.77 mwaka 2025/2026, hadi tani 80,000 mwaka 2026/2027,” amesema.
Akizungumzia utekelezaji wa bajeti iliyopita ya Mwaka 2025/2026, amesema Bodi imefanikiwa kutekeleza yaliyoainisha katika bajeti hiyo na mengine yanaendelea kutekelezwa ambapo imefanikiwa kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja ya Mkonge ya wakulima wadogo yenye ukubwa wa hekta 9,211 katika mikoa ya Morogoro (hekta 1,519), Pwani (hekta 343), Tanga (hekta 6,411) na Kilimanjaro (hekta 938).
“Aidha, Bodi imeendelea kuwezesha umiliki wa ardhi ya kilimo yenye ukubwa wa hekta 21,625.5 katika mikoa ya Tanga (hekta 16,027.50), Morogoro (hekta 3,797.50) na Arusha (hekta 1,800). Mashamba hayo yanatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mkonge tani 120,000 ifikapo mwaka 2030.
“Wizara kupitia Bodi ya Mkonge katika mwaka 2025/2026, ilipanga kuhamasisha wakulima kuongeza uzalishaji wa zao la Mkonge kufikia tani 80,000 kutoa mafunzo ya uongezaji thamani wa mkonge; kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja yenye ukubwa wa hekta 2,000; kuwezesha umiliki wa ardhi ya kilimo yenye ukubwa wa hekta 6,000; kuanzisha Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkonge; kununua na kusimika mashine 10 za kuchakata mkonge (dikotiketa); kurejesha viwanda na mashamba yaliyokuwa chini ya kampuni ya Sisalana; na kuendelea na ujenzi wa kituo cha uzalishaji wa nzi chuma,” amesema Mhe. Chongolo.
Pamoja na mambo mengine ameelezea uwezeshaji vijana na wanawake kuongeza thamani ya mazao . Wizara ilipanga kutekeleza mradi wa BBT kwa vijana na wanawake 200 kwa kuwapatia mafunzo ya kuongeza thamani ya zao la Mkonge ili waweze kuzalisha bidhaa zitokanazo na zao hilo.
“Ninaomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa hadi Machi 2026, mafunzo atamizi kuhusu uongezaji thamani wa zao la Mkonge yametolewa kwa vijana na wanawake 352 wakiwamo wanawake 305 na wanaume 47 kupitia programu ya Mkonge BBT kwa upande wa Zanzibar na Mkoa wa Tanga vijana na wanawake hao wamewezeshwa mashine 20 na tani tisa za Mkonge kwa ajili ya kutengeneza bidhaa,” amesema.








